26.The Poets

  1. «Ṭā, Sīn, Mīm.» Yametangulia maelezo kuhusu herufi za mkato mwanzo wa sura ya Al-Baqarah
  2. Hizi ni aya za Qur’ani yenye kufafanua kila kitu, yenye kupambanua baina ya uongofu na upotevu
  3. Huenda wewe, ewe Mtume, kwa kuwa una hamu sana ya kutaka wao waongoke, ukajiangamiza mwenyewe kwa kuwa wao hawakukuamini na hawakufuata kimatendo uongofu wako. Basi usifanye hivyo
  4. Tukitaka tutawateremshia wakanushaji, miongoni mwa watu wako, miujiza itokayo mbinguni yenye kuwaogopesha itakayowalazimisha wao kuamini, na hapo shingo zao ziwe zimenyongeka na kudhalilika. Lakini hatukutaka hilo, kwani Imani yenye kunufaisha ni kuyaamini yaliyoghibu kwa hiyari
  5. Na hauwajii washirikina hawa ukumbusho, kutoka kwa Mwingi wa rehema unaoanzwa kuteremshwa, kitu baada ya kitu, wenye kuwaamrisha na kuwakataza na kuwakumbusha Dini ya kweli, isipokuwa wanaupa mgongo na hawaukubali
  6. Kwa hakika washaikanusha Qur’ani na washaifanyia shere, basi zitawajia wao habari za jambo ambalo walikuwa wakilifanyia shere na dharau, na itawashukia wao adhabu ikiwa ni malipo ya kumuasi Mola wao
  7. Je, wanakanusha na hali wao hawakuiangalia ardhi ambayo ndani yake tumeotesha kila aina nzuri ya mimea ambayo hakuna awezae kuiyotesha isipokuwa Mola wa viumbe vyote
  8. Kwa hakika, katika kuitoa mimea kwenye ardhi ni dalili wazi ya ukamilifu wa uweza wa Mwenyezi Mungu, na wengi wa watu hawakuwa ni wenye kuamini
  9. Na kwa hakika Mola wako Ndiye Mshindi wa kila kiumbe, ni Mwenye kurehemu Ambaye rehema Yake imeenea kila kitu
  10. Na wakumbushe watu wako, ewe Mtume, pindi Mola wako Alipomuita Mūsā kuwa awaendee watu madhalimu
  11. nao ni watu wa Fir’awn na uwaambie wayaogope mateso ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na waache ukafiri na upotevu walionao
  12. Mūsā akasema, «Mola wangu! Mimi ninaogopa wasije wakanikanusha juu ya utume
  13. na moyo wangu ukaingia kero kwa kunikanusha, na ulimi wangu usiwe na ufasaha wa kulingania. Basi mtume Jibrili aende na wahyi kwa ndugu yangu Hārūn, ili anisaidie na aniamini kwa ninayoyasema, na awafafanulie kile ninachowaambia, kwani yeye ana ufasaha zaidi wa matamshi kuliko mimi
  14. Na watanishika na kosa la kumuua mwanamume wa jamii ya Qibṭī miongoni mwao, na kwa hivyo ninaogopa wasiniue kwa ajili yake.»
  15. Mwenyezi Mungu Akamwambia Mūsā, «Sivyo hivyo! Hawatakuua. Na nimekubali matakwa yako juu ya Hārūn. Basi endeni mkiwa na miujiza yenye kuonyesha ukweli wenu. Sisi tuko pamoja na nyinyi kwa ujuzi, utunzi na usaidizi tunasikiliza
  16. Mjieni Fir’awn na mumwambie, «Sisi tumetumwa kwako na kwa watu wako kutoka kwa Mola wa viumbe wote
  17. kwamba uwaache Wana wa Isrāīl waende na sisi.»
  18. Fir’awn akasema kumwambia Mūsā kwa kumsimanga, «Je, hatukukulea kwenye majumba yetu ukiwa mchanga, ukakaa kwenye utunzi wetu miaka (mingi) katika umri wako
  19. ukafanya tendo la jinai kwa kumuua mwanamume miongoni mwa watu wangu, ulipompiga na ukamsukuma, na wewe ni miongoni mwa wakanushaji neema zangu na kukataa uola wangu
  20. Mūsā akasema kumjibu Fir’awn, «Nilifanya uliyoyataja kabla Mwenyezi Mungu Hajaniletea wahyi na kunitumiliza kama Mtume
  21. ndipo nilitoka kwenu kwa kukimbia kuelekea Madyan nilipoogopa usije ukaniua kwa nililolifanya bila kukusudia, Na Mola wangu Akanitunuku unabii na elimu na Akanifanya ni miongoni mwa Mitume
  22. Na kwani huko kulelewa nyumbani kwako unakuona ni neema kutoka kwako juu yangu, na hali wewe umewafanya Wana wa Isrāīl ni watumwa , unawachinja wana wao wa kiume na unawaachilia wanawake wao ili watumwe na wadharauliwe?»
  23. Fir’awn akamwambia Mūsā, «Na huyo Mola wa viumbe wote Ambaye unadai kwamba wewe ni mjumbe Wake, ni kitu gani?»
  24. Mūsā akasema, «Yeye ni Mmiliki na Mwenye kuipelekesha mbingu na ardhi na vilivyoko baina ya viwili hivyo. Iwapo nyinyi mna yakini na hilo, basi aminini.»
  25. Fir’awn akasema kuwaambia walioko pambizoni mwake miongoni mwa watukufu wa watu wake, «Je, hamusikii maneno ya Mūsā ya ajabu kwamba kuna mola asiyekuwa mimi?»
  26. Mūsā akasema, «Mola Ambaye mimi nawalingania nyinyi Kwake ni Yule Aliyewaumba nyinyi na Aliyewaumba wa mwanzo. Basi vipi nyinyi mnamuabudu ambaye ni kiumbe kama nyinyi na yeye ana mababa waliotoeka kama mababa zenu?»
  27. Fir’awn akasema kuwaambia wale watu wake makhsusi akiwapandisha ghadhabu zao, kwa kuwa Mūsā amemkanusha yeye, «Kwa kweli, huyu mjumbe wenu aliyeletwa kwenu ni mwendawazimu , asema maneno yasiyofahamika.»
  28. Mūsā akasema, «Mola wa Mashariki na Magharibi na vilivyoko baina ya viwili hivyo, na vilivyomo ndani yake vya mwangaza na giza. Hili linapelekea kuwa ni lazima kumuamini Yeye Peke Yake, iwapo nyinyi ni miongoni mwa watu wa akili na kuzingatia.»
  29. Fir’awn akamwambia Mūsā kwa kumtisha, «Ukichukua mwingine aseyekuwa mimi ukamfanya ni mola nitakufunga jela pamoja na wale niliowafunga.»
  30. Mūsā akasema, «Je, utanifanya mimi ni miongoni mwa wafungwa jela, hata nikikuletea hoja ya kukata ambayo kwa hiyo utabainika ukweli wangu?»
  31. Fir’awn akasema, «Basi ilete ikiwa wewe ni miongoni mwa wakweli katika madai yako.»
  32. Hapo Mūsā akaitupa fimbo yake na ikageuka kuwa nyoka wa kikweli, si kiinimacho kama wanavyofanya wachawi
  33. Na akautoa mkono wake kwenye uwazi wa kanzu yake uliofunguliwa kifuani au chini ya kwapa lake, na papo hapo ukawa mweupe kama barafu, na sio weupe wa mbalanga, ukawashangaza waangaliaji
  34. Fir’awn akasema kuwaambia watukufu wa watu wake, kwa kuogopa wasije wakaamini, «Kwa kweli Mūsā ni mchawi hodari
  35. Anataka kuwatoa nyinyi, kwa uchawi wake, kwenye ardhi yenu. Basi mnatoa shauri gani kuhusu yeye nipate kuyafuata maoni yenu?»
  36. Watu wake wakamwambia, «Msubirishe Mūsā na Hārūn, na utume askari mijini wawakusanye wachawi
  37. Watakujia na kila anayejua uchawi na akawa hodari kuufahamu.»
  38. Wakakusanywa wachawi, na wakapangiwa wakati maalumu, nao ni wakati wa mchana wa siku ya Pambo ambayo wanajitenga na shughuli zao, na wanajikusanya na kujipamba, ili wakutane na Mūsā
  39. na wawahimize watu kujumuika kwa matarajio kwamba ushindi uwe ni wa wachawi
  40. Sisi tunatarajia ushindi uwe ni wa wachawi ili tujikite kwenye dini yetu
  41. Na wachawi walipomjia Fir’awn walimwambia, ‘Je, sisi tutakuwa na malipo ya mali au heshima ikiwa tutakuwa ni wenye kumshinda Mūsā?»
  42. Fir’awn akasema, «Ndio, nyinyi mtapata kwangu malipo mnayoyataka, na nyinyi hapo mtakuwa ni miongoni mwa wenye kusogezwa karibu na mimi.»
  43. Mūsā akasema kuwaambia wachawi, akitaka kuutangua uchawi wao na kuonyesha kuwa kile alichokileta si uchawi, «Tupeni mtakavyovitupa vya uchawi.»
  44. Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na zikawadhihirikia watu kwenye akili zao kuwa ni nyoka wanaotembea, na wakaapa kwa enzi ya Fir’awn kwa kusema, «Sisi ni wenye kushinda.»
  45. Hapo akaitupa Mūsā fimbo yake, na papo hapo ikawa ni nyoka mkubwa, akawa anavimeza vile vilivyotokana na wao, hao wachawi, vya uzushi na bandia
  46. Waliposhuhudia hilo na wakajua kuwa halitokani na udanganyifu wa wachawi, walimuamini Mwenyezi Mungu na wakamsujudia
  47. na wakasema, «Tumemuamini Mola wa viumbe vyote
  48. Mola wa Mūsā na Hārūn.»
  49. Fir’awn akasema kuwaambia wachawi kwa kukataa, «Mumemkubali Mūsā bila ya idhini yangu!» Na akasema akiashiria kuwa kitendo cha Mūsā ni uchawi, «Yeye ni mkubwa wenu aliyewafundisha nyinyi uchawi, basi mtayajua mateso yatakayowafikia. Nitaikata mikono yenu na miguu yenu kitafauti: kwa kuukata mkono wa kulia na mguu wa kushoto au kinyume chake, na nitawasulubu nyote.»
  50. Wachawi walisema kumwambia Fir’awn, «Hakuna madhara ya duniani yatakayotupata, kwa kweli sisi ni wenye kurudi kwa Mola wetu, Atupe neema ya kuendelea
  51. Sisi tunataraji Mola wetu Atusamehe makosa yetu ya ushirikina na mengineyo kwa kuwa sisi ndio Waumini wa mwanzo katika watu wako.»
  52. Na Mwenyezi Mungu Akampelekea wahyi Mūsā, amani imshukie, kwamba, «Enda usiku pamoja na walioamini miongoni mwa Wana wa Isrāīl, ili Fir’awn na askari wake, ambao watawafuata nyinyi, wasije wakawafikia kabla ya kufika kwenu baharini.»
  53. Fir’awn akawatuma askari wake, alipopata habari kwamba Wana wa Isrāīl wameenda usiku, wakusanye jeshi lake kutoka miji ya utawala wake
  54. Fir’awn akasema, «Kwa kweli, Wana wa Isrāīl waliokimbia pamoja na Mūsā ni pote twevu lenye idadi ndogo
  55. Na wao wamevijaza hasira vifua vyetu kwa kuwa wameenda kinyume na dini yetu na wametoka bila ya idhini yetu
  56. na sisi sote tuko macho, tuko tayari nao.»
  57. Mwenyezi Mungu Akamtoa Fir’awn na watu wake kwenye ardhi ya Misri yenye mabustani, mabubujiko ya maji
  58. hazina za mali na majumba mazuri
  59. Na kama tulivyowatoa, tuliwapatia nyumba hizo Wana wa Isrāīl baada yao wao
  60. Hivyo basi Fir’awn na askari wake walimkuta Mūsā na waliokuwa pamoja na yeye wakati wa kuchomoza jua
  61. Yalipoonana makundi mawili, watu wa Mūsā walisema, «Kwa hakika jumuiko la Fir’awn ni lenye kutufikia na kutuangamiza.»
  62. Mūsā alisema kuwaambia, «Sivyo! Mambo si kama mlivyotaja. Hamtafikiwa. Kwa hakika Mwenyezi Mungu Yupo na mimi kwa msaada, Ataniongoza njia ya kuokoka mimi na kuokoka nyinyi.»
  63. Hapo tukampelekea wahyi Mūsā kwamba, «Piga bahari kwa fimbo yako!» Akapiga. Na bahari ikapasuka njia kumi na mbili kwa idadi ya kabila za Wana wa Isrāīl. Na kila kipande kilichojitenga na bahari ni kama jabali kubwa
  64. Na tulimsogeza karibu Fir’awn na watu wake mpaka wakaingia baharini
  65. Na tukamuokoa Mūsā na waliokuwa pamoja na yeye wote. Bahari ikaendelea kuachana kwake (kwa ule mpasuko) mpaka wakavuka kwenye nchi kavu
  66. Kisha tukamzamisha Fir’awn na waliokuwa pamoja na yeye kwa kuifanya bahari iwafinike baada ya wao kuingia ndani wakimfuata Mūsā na watu wake
  67. Kwa hakika, katika hilo lililotukia pana mazingatio ya ajabu yenye kuonyesha dalili ya uweza wa Mwenyezi Mungu. Na wengi wa wafuasi wa Fir’awn hawakuwa ni wenye kuamini, pamoja na alama hii yenye kushinda
  68. Na hakika ya Mola wako Ndiye Mshindi, Ndiye Mwenye kurehemu. Kwa nguvu Zake na ushindi Amewaangamiza makafiri wakanushaji, na kwa rehema Yake Amemuokoa Mūsā na waliokuwa pamoja na yeye wote
  69. Na wasimulie makafiri, ewe Mtume, habari ya Ibrāhīm
  70. alipomwambia babake na watu wake, «Mnaabudu kitu gani?»
  71. Wakasema, «Tunaabudu masanamu, tunaketi na kuendelea kuwaabudu.»
  72. Akasema Ibrāhīm akiwatanabahisha uharibifu wa njia yao, «Kwani wanasikia maombi yenu mnapowaomba
  73. Au wanawapatia manufaa mkiwaabudu? Au wanawafanya mupate madhara mkiacha kuwaabudu?»
  74. Wakasema, «Haliwi lolote katika hayo, lakini tuliwakuta mababa zetu wakiwaabudu, na sisi tukawaiga katika yale ambayo walikuwa wakiyafanya.»
  75. Ibrāhīm akasema, «Je, mumefikiria kuvitia akilini hivyo mnavyoviabudu, miongoni mwa masanamu yasiyosikia wala kunufaisha wala kudhuru
  76. nyinyi na mababa zenu waliowatangulia
  77. Kwani hao mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni maadui zangu. Lakini Mola wa viumbe wote na Mmiliki wa mambo yao, Yeye Peke Yake Ndiye ninayemuabudu
  78. Yeye Ndiye Aliyeniumba kwa sura nzuri zaidi. Yeye ananiongoza kwenye maslahi ya dunia na Akhera
  79. Na Yeye Ndiye Anayenineemesha kwa chakula na kinywaji
  80. Na nikipatikana na ugonjwa, Yeye Ndiye Anayeniponyesha na kuniondolea
  81. Na Yeye Ndiye Atakayenifisha duniani kwa kuichukua roho yangu, kisha Atanihuisha Siku ya Kiyama, hakuna awezaye hilo isipokuwa Yeye
  82. Na Ambaye ninatarajia Atanisamehe dhambi zangu Siku ya Malipo.»
  83. Ibrāhīm akasema akimuomba Mola wake, «Mola wangu! Nitunukie elimu na fahamu, na unikutanishe na watu wema, na unikusanye mimi na wao Peponi
  84. «Na unifanye niwe na sifa nzuri na utajo mwema kwa wale watakaokuja baada yangu mpaka Siku ya Kiyama
  85. «Na unifanye mimi niwe miongoni mwa waja wako utakaowarithisha starehe za Peponi.»
  86. Hii ni dua ya Ibrāhīm, amani imshukiye, ya kumuomba Mwenyezi Mungu Amuokoe babake na upotevu na Ampe uongofu, ili Amghufirie na Amsamehe, kama Ibrāhīm alivyomuahidi babake kumuombea Mungu, na ilipomfunukia kuwa yeye ni mwenye kuendelea kwenye ukafiri na ushirikina mpaka afe alijiepusha naye
  87. «Na usinipe unyonge Siku hiyo, ambayo watu watatoka makaburini ili wahesabiwe na walipwe
  88. Siku ambayo mali na watoto havitamfaa yoyote miongoni mwa waja
  89. isipokuwa yule aliyemjia Mwenyezi Mungu kwa moyo uliyosalimika na ukafiri, unafiki na uovu.»
  90. Na Pepo itasogezwa karibu kwa wale waliojiepusha na ukafiri na matendo ya uasi na wakamuelekea Mwenyezi Mungu kwa kumtii
  91. Na Moto utaonyeshwa waziwazi kwa makafiri ambao walipotea njia ya uongofu na wakayafanyia ujasiri yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu na wakawakanusha Mitume Wake
  92. Na wataambiwa kwa kulaumiwa, «Wako wapi waungu wenu ambao mlikuwa mkiwaabudu
  93. badala ya Mwenyezi Mungu na mkidai kwamba wao watawaombea leo? Je, watawanusuru na wawazuilie adhabu isiwafikie au watajinusuru kwa kuikinga adhabu isiwafikie?» Hakuna chochote katika hayo
  94. Hapo watakusanywa na watupwe kwenye Jahanamu kwa vichwa vyao, mara baada ya nyingine mpaka watakapotulia humo: wao, wale waliowapoteza
  95. na wasaidizi wa Iblisi waliowapambia shari; hakuna yoyote kati yao atakayeponyoka
  96. Watasema wakikiri makosa yao, na huku wanagombana, ndani ya Jahanamu, na wale waliowapoteza wao
  97. «Tunaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba sisi, duniani, tulikuwa kwenye upotevu ulio waziwazi, haukuwa umefichika
  98. tulipowafanya nyinyi kuwa ni sawa na Mola wa viumbe wote, Anayestahiki kuabudiwa, Peke Yake
  99. Na hakuna kilichotutia kwenye mwisho huu mbaya isipokuwa ni wahalifu ambao walitulingania tumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu
  100. «Hapana yoyote wa kutuombea na kututoa kwenye adhabu
  101. wala mwenye kutupenda kikweli na kutuhurumia
  102. «Tunatamani tupatiwe fursa ya kurudi ulimwenguni tupate kuwa miongoni mwa wenye kuamini na kuokolewa.»
  103. Hakika katika habari ya Ibrāhīm iliyotangulia kuna mazingatio kwa mwenye kuzingatia. Na wengi wenye kuisikia habari hii hawakuwa ni wenye kuamini
  104. Na kwa hakika, Mola wako Ndiye Mshindi Aliye Muweza wa kuwalipiza wakanushaji, Ndiye Mwenye kuwarehemu waja Wake Waumini
  105. Waliukanusha watu wa Nūḥ ujumbe wa Nabii wao. Wakawa, kwa kufanya hivyo, ni wakanushaji wa Mitume wote, kwa kuwa kila Mtume anaamrisha kuwaamini Mitume wote
  106. Kumbuka pindi aliposema kuwaambia wao ndugu yao Nūḥ, «Je, hamumuogopi Mwenyezi Mungu kwa kuacha kumuabudu asiyekuwa Yeye
  107. Mimi kwenu nyinyi ni Mtume muaminifu katika yale ninayowafikishia
  108. Basi ifanyeni Imani kuwa ndio kinga yenu na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na nitiini mimi katika yale ninayowaamrisha ya kumuabudu Yeye Peke Yake
  109. na sitaki kutoka kwenu malipo yoyote ya kuufikisha ujumbe, malipo yangu hayako juu ya yoyote isipokuwa Mola wa viumbe wote, Mwenye kuendesha mambo ya viumbe Vyake
  110. Basi jihadharini na mateso Yake na mnitii mimi kwa kufuata amri Zake na kujiepusha na makatazo Yake.»
  111. Watu wake wakamwambia, «Vipi tutakuamini na tutakufuata na hali hao waliokufuata ni watu wanyonge na wale wa hali ya chini miongoni mwao?»
  112. Nūḥ, amani imshukie, aliwajibu kwa kusema, «Sikupewa jukumu la kujua matendo yao. Jukumu nililopewa ni kuwalingania wao kwenye Imani. Na linalozingatiwa ni Imani, na sio cheo, ukoo, kazi na ujuzi wa sanaa
  113. «Hesabu yao, ili walipwe kwa matendo yao na yaliyomo ndani ya nafsi zao, ni juu ya Mola wangu Anayeona na kujua siri zote. Lau mnatambua hilo hamngalisema maneno haya
  114. «Na mimi si mwenye kuwafukuza wale wanaouamini ulinganizi wangu, namna itakavyokuwa hali yao, kwa kufuata matakwa yenu, ili mniamini
  115. Mimi sikuwa isipokuwa ni mwonyaji ambaye onyo lake liko wazi.»
  116. Hapo watu wa Nūḥ waliacha kubishana na wakaamua kutoa vitisho, hivyo basi wakamuambia, «Usiporudi nyuma, ewe Nūḥ, ukaacha huo ulinganizi wako, utakuwa ni miongoni mwa wenye kuuawa kwa kupigwa mawe.»
  117. Nūḥ aliposikia neno lao hili, alimuomba Mola wake kwa kusema, «Mola wangu! Kwa hakika watu wangu wameamua kuendelea kunikanusha
  118. basi amua baina yangu na wao uamuzi wa kumwangamiza mwenye kukataa kukupwekesha na akamkanusha Mtume wako. Na uniokoe mimi, na Waumini walio pamoja na mimi, na adhabu utakayowaadhibu makafiri.»
  119. Basi tukamuokoa na wale walio pamoja na yeye katika jahazi iliyojazwa aina mbalimabali za viumbe alivyovibeba pamoja na yeye
  120. Kisha tukawazamisha, baada ya kumuokoa Nūḥ na wale waliokuwa pamoja na yeye, wale waliosalia kati ya wale ambao hawakuamini na wakaukataa ushauri aliyowapa
  121. Hakika katika maelezo ya Nūḥ na yale yaliyokuwa ya kuokolewa Waumini na kuangamizwa wakanushaji ni alama na ni zingatio kubwa kwa waliokuja baada yao. Na wengi wa wale waliokisikia kisa hiki hawakuwa ni wenye kumuamini Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na sheria Zake
  122. Na kwa kweli Mola wako Ndiye Mshindi katika kuwatesa waliomkanusha na wakaenda kinyume na amri Yake, Mwenye rehema kwa waja Wake walioamini
  123. Walimkanusha watu wa kabila la ‘Ād Mtume wao Hūd, amani imshukiye, na kwa hivyo wakawa ni wakanushaji wa Mitume wote, kwa kuwa ulinganizi wao ni mmoja katika misingi yake na malengo yake
  124. Alipowaambia ndugu yao Hūd, «Je, hamumchi MwenyeziMungu mukamtakasia ibada
  125. Mimi nimetumwa kwenu niwaongoze na niwaonyeshe njia, ni mtunzi wa ujumbe wa Mwenyezi Mungu, ninaufikisha kwenu kama Alivyoniamrisha Mola wangu
  126. Basi iogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu na mnitii mimi katika kile ninachowaitia nyinyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu
  127. na sitaki kutoka kwenu, kwa kuwaongoza nyinyi kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu, aina yoyote ya malipo. Malipo yangu hayako juu ya yoyote isipokuwa Mola wa viumbe wote
  128. «Je mnajenga kila mahali palipoinuka jengo refu mkawa mnatazama kutoka hapo na mnawacheza shere wapita njia? Huo ni upuuzi na upitaji kiasi, na hauwaletei nyinyi faida yoyote katika dini au katika dunia
  129. Na mnafanya majumba imara na ngome zilizojengwa madhubuti, kama kwamba nyinyi mtakaa milele duniani na hamtakufa
  130. Na mnapomshika mtu kwa nguvu na mkamakinika kumuua au kumpiga, basi mnalifanya hilo kwa kutendesha nguvu hali ya kufanya maonevu
  131. «Basi muogopeni Mwenyezi Mungu na mkifuate kile ninachowalingania, kwani hilo lina nafuu zaidi kwenu
  132. na mcheni Mwenyezi Mungu Aliyewapa aina mbalimbali za neema zisizofichika kwenu
  133. Amewapa wanyama hawa: ngamia ng’ombe, mbuzi na kondoo, na Amewapa watoto
  134. na Amewapa mabustani yenye matunda, na Amewatolea maji kwenye chemchemi zinazopita
  135. Hūd, amani imshukiye, akasema akiwatahadharisha wao, «Mimi ninaogopa , mkiendelea na yale mliyo nayo ya ukanushaji, uonevu na kuzikufuru neema, asije Mwenyezi Mungu Akawateremshia nyinyi adhabu katika Siku ambayo shida yake ni kubwa kwa kitisho cha adhabu yake
  136. Wakamwambia, «Ni sawa kwetu kutukumbusha, kututisha na kuacha kufanya hivyo, hatutakuamini
  137. Na wakasema, «Haikuwa dini hii tuliyonayo isipokuwa ni dini ya watu wa mwanzo na desturi zao
  138. na sisi si wenye kuadhibiwa kwa tunalolifanya katika yale ambayo unatuonya nayo ya adhabu.»
  139. Wakaendelea kumkanusha, na Mwenyezi Mungu Akawaangamiza kwa upepo wa baridi ulio mkali. Kwa hakika, katika kuangamiza huko kuna mazingatio kwa wanaokuja baada yao, na hawakuwa wengi wao, wale waliokisikia kisa chao, ni wenye kukuamini wewe
  140. Hakika Mola wako Ndiye Mwenye nguvu, Mshindi kwa anayoyataka ya kuwaangamiza wakanushaji, Mwenye huruma kwa Waumini
  141. Watu wa kabila la Thamūd waliukanusha ujumbe wa Mtume wao Ṣāliḥ na wakaukanusha mwito wake wa kumpwekesha Mwenyezi Mungu, na kwa hivyo wakawa wamewakanusha Mitume wote, kwa kuwa wao wote wanalingania kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu
  142. Pindi alipowaambia wao ndugu yao Ṣāliḥ»Je, hamuogopi mateso ya Mwenyezi Mungu, mkampwekesha kwa ibada
  143. Mimi nimetumilizwa kwenu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ni mwenye kuutunza ujumbe huu kama nilivyoupokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu
  144. Basi jihadharini na mateso Yake, Aliyetukuka, na fuateni kile nilichowalingania mkifuate
  145. Na mimi sitaki malipo kwa kuwashauri na kuwaongoza, malipo yangu hayako isipokuwa kwa Mola wa viumbe wote
  146. «Je, Awaache Mola wenu katika starehe mlizonazo, hali ya kuwa mumetulia katika dunia hii mkiwa mumesalimika na adhabu na kuondoka na kufa
  147. Mkiwa kwenye mabustani yenye matunda, chemchemi zinazopita
  148. nafaka nyingi na mitende ambayo matunda yake yamestawi, yamelainika na yameiva
  149. na mnachonga kutoka kwa majabali majumba hali ya kuwa ni wamahiri wa kuyachonga, mkiwa na kiburi na majivuno.»
  150. Basi ogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu na mkubali ushauri wangu
  151. na msiandame amri ya wenye kuzidhulumu nafsi zao, waliokolea katika kumuasi Mwenyezi Mungu
  152. waliozoea kufanya uharibifu kwenye ardhi, uharibifu usiotengenezeka
  153. Watu wa Thamūd walimwambia Nabii wao Ṣāliḥ, «Wewe hukuwa isipokuwa ni miongoni mwa wale waliofanyiwa uganga wa uchawi mwingi, mpaka uchawi ukaathiri akili yako
  154. Hukuwa wewe isipokuwa ni mmoja wa wanadamu unaofanana na sisi katika ubinadamu, basi vipi utakuwa tafauti na sisi kwa utume? Basi leta hoja wazi inayoonyesha kuwa utume wako umethibiti, iwapo wewe ni mkweli katika madai yako kwamba Mwenyezi Mungu Amekutumiliza kwetu.»
  155. Ṣāliḥ akasema kuwaambia- na hapo alikuwa amewaletea ngamia ambaye Mwenyezi Mungu alimtolea kwenye jiwe-, «Huyu ni ngamia wa Mwenyezi Mungu. Yeye ana hisa ya maji siku maalumu, na nyinyi mna hisa ya maji kwa siku nyingine. Haifai kwenu nyinyi kunywa siku ile ambayo ni hisa yake, na yeye hatakunywa siku ambayo ni hisa yenu
  156. Na msimguse kwa kitu chochote cha kumdhuru, kama kipigo au mauaji au mfano wake, kwani mkifanya hivyo, Mwenyezi Mungu Atawaangamiza nyinyi kwa adhabu ya Siku ambayo shida yake ni kubwa kwa sababu ya papatiko litakalotukia Siku hiyo na shida
  157. Basi wakamchinja ngamia, wakawa ni wenye kujuta kwa walilolifanya walipokuwa na uhakika kuwa watashukiwa na adhabu, na majuto yao yasiwafae kitu
  158. Basi adhabu ya Mwenyezi Mungu ikawashukia, ile ambayo Ṣāliḥ, amani imshukiye, aliwaahidi nayo, na ikawaangamiza. Kwa hakika, katika kuwaangamiza watu wa Thamūd pana mazingatio kwa mwenye kuuzingatia mwisho huu; na wengi wao hawakuwa ni wenye kuamini
  159. Na kwa hakika Mola wako Ndiye Mshindi, Mwenye kutendesha nguvu, Mwenye kuwatesa maadui Wake, Mwenye huruma kwa walioamini miongoni mwa viumbe Wake
  160. watu wa Lūṭ waliukanusha utume wake, wakawa kwa hilo ni wakanushaji wa Mitume waliosalia, kwa kuwa lile walilolileta la kumpwekesha Mwenyezi Mungu na misingi ya Sheria ni moja
  161. Pindi ndugu yao Lūṭ alipowaambia, «Je, hamuogopi adhabu ya Mwenyezi Mungu
  162. Mimi ni mjumbe kutoka kwa Mola wenu aliye muaminifu juu ya utekelezaji wa ujumbe Wake kwenu
  163. Basi jihadharini na mateso ya Mwenyezi Mungu kwa kumkanusha kwenu mjumbe Wake, na nifuateni mimi katika yale ninayowalingania
  164. Na siwaombi malipo yoyote juu ya ulinganizi wangu wa kuwaongoza, malipo yangu hayako isipokuwa kwa Mola wa viumbe wote
  165. «Mnawaingilia binadamu wanaume
  166. na mnawaacha wake zenu ambao Mwenyezi Mungu Amewaumbia nyinyi ili mstarehe na mzaane? Lakini nyinyi ni watu, kwa uasi huu, wenye kuyakiuka yale ambayo Mwenyezi Mungu Amewaruhusu ya halali na kuyaendea ya haramu.»
  167. Watu wa Lūṭ wakasema, «Usipoacha, ewe Lūṭ, kutukataza kuwajia wanaume na kukichafua kitendo hicho (cha kuwajia wanaume), utakuwa ni miongoni mwa wenye kufukuzwa kutoka miji yetu.»
  168. Lūṭ akasema kuwaambia wao, «Mimi ni miongoni mwa wale wanaokichukia sana kitendo chenu mnachokifanya cha kuwajia wanaume.»
  169. Kisha Lūṭ akamuomba Mola wake, alipokata tamaa kuwa watamsikiliza, alisema, «Mola wangu! Niokoe mimi na uwaokoe jamaa zangu na kile wanachokifanya watu wangu cha uasi huu mchafu na (utuokoe na) adhabu yako itakayowapata.»
  170. Basi tukamuokoa yeye na watu wa nyumbani kwake na wale wote walioukubali ulinganizi wake
  171. isipokuwa mkongwe miongoni mwa watu wa nyumbani kwake, naye ni mke wake ambaye hakushirikiana na wao katika kuamini, hivyo basi akawa ni mwenye kusalia kwenye adhabu na maangamivu
  172. Kisha tukawaangamiza wasiokuwa wao, miongoni mwa makafiri, kuwaangamiza kukubwa
  173. na tukawateremshia wao mawe kutoka juu kama mvua yakawaangamiza. Ilikuwa mvua mbaya sana ya wale walioonywa na Mitume wao na wasiwakubalie. Kwa hakika, wao wameteremshiwa aina mabaya zaidi za maangamivu na uvunjaji
  174. Kwa hakika, katika mateso hayo yaliyowateremkia watu wa Lūṭ pana mazingatio na mawaidha ya kuwafanya wenye kukanusha wawaidhike. Na wengi wao hawakuwa ni wenye kuamini
  175. Na kwa kweli Mola wako Ndiye Mshindi Mwenye nguvu ya kuweza kuwashurutisha wakanushaji, Mwenye huruma kwa waja Wake wema
  176. Walimkanusha watu wa nchi yenye miti iliyoshikana Mtume wao Shu’ayb kuhusu utume wake, na kwa hivyo waliukua wamekanusha jumbe zote za Mitume
  177. Alipowaambia wao Shu’ayb, «Je, hamuogopi kuwa Mwenyezi Mungu Atawatesa kwa ushirikina wenu na kufanya kwenu matendo ya uasi
  178. Mimi nimetumilizwa kwenu kutoka kwa Mwenyezi Mungu niwaongoe, ni mtunzi wa kile alichoniletea mimi Mwenyezi Mungu cha wahyi wa utume
  179. Basi yaogopeni mateso ya Mwenyezi Mungu na mkifuate kile ninachowaitia cha uongofu wa Mwenyezi Mungu mupate kuongoka
  180. Na sitaki kwenu, kwa kule kuwalingania kwangu kwenye kumuamini Mwenyezi Mungu, malipo yoyote. Malipo yangu hayako isipokuwa kwa Mola wa viumbe wote.”
  181. Shu’ayb akaendelea kuwaambia- na walikuwa wakipunguza vipimo na mizani-, «Watimizieni watu vipimo kwa kuwakamilishia, na msiwe ni kati ya wale wanaowapunja watu haki zao
  182. na mpime kwa mizani ya uadilifu iliyolingana sawa
  183. na msiwapunje watu chochote katika haki zao kwenye vipimo au mizani au vinginevyo, na msizidishe uharibifu katika ardhi kwa kufanya ushirikina, kuua, kunyang’anya, kuwatisha watu na kutekeleza vitendo vya uasi
  184. «Na jihadharini na mateso ya Mwenyezi Mungu Aliyewaumba na Akawaumba watu wa mataifa yaliyowatangulia.»
  185. Wakasema, «Ukweli ni kwamba wewe, ewe Shu’ayb, ni miongoni mwa wale waliopatwa na uchawi ukawashika sana ukawaondoa akili zao
  186. Na wewe hukuwa isipokuwa ni mfano wetu sisi katika ubinadamu, basi vipi utahusika peke yako kwa utume bila ya sisi? Na kwa kweli, dhana yetu kubwa kuhusu wewe ni kuwa wewe ni miongoni mwa warongo katika kile unachokidai cha utume
  187. Iwapo wewe ni mkweli katika madai yako ya utume, basi muombe Mwenyezi Mungu Atuangushie vipande vya adhabu kutoka mbinguni vitumalize.»
  188. Shu’ayb akawaambia wao, «Mola wangu Anayajua zaidi yale mnayoyafanya ya ushirikina na uasi na mateso mnayostahili.»
  189. Wakaendelea kumkanusha, likawapata wao joto kali, wakawa wanatafuta mahali pa hifadhi ili wajifinike. Kikawafinika kiwingu, kikawapatia ubaridi na upepo laini, na walipokusanyika chini yake, moto uliwawakia na ukawachoma, basi hapo yakawa maangamivu yao wote katika siku yenye kitisho kikali
  190. Hakika katika mateso hayo yaliyowashukia kuna ushahidi wazi juu ya uweza wa Mwenyezi Mungu katika kuwapatiliza wakanushaji kwa adhabu na kuna mazingatio kwa mwenye kuzingatia. Na hawakuwa wengi wao ni wenye kuamini na kuwaidhika kwa hayo
  191. Na kwa hakika, Mola wako, ewe Mtume, Ndiye Yeye Aliye Mshindi katika kuwatesa Kwake wale Anaowatesa miongoni mwa maadui Wake, Ndiye Anayewarehemu waja Wake wanaompwekesha
  192. Na kwa hakika, hii Qur’ani ambayo ndani yake zimetajwa habari hizi za kweli imeteremshwa na Muumba viumbe na Mmiliki wa mambo yote
  193. Jibrili muaminifu ameshuka nayo
  194. akakusomea mpaka ukaikusanya moyoni mwako, kwa kuihifadhi na kuielewa, upate kuwa ni mmoja wa wajumbe wa Mwenyezi Mungu wenye kuwafanya watu wao waogope mateso ya Mwenyezi Mungu, upate kuwaonya, kwa Teremsho hili, binadamu na majini wote
  195. Ameshuka nayo Jibrili kwako kwa lugha ya Kiarabu yenye maana yaliyo wazi, yenye ushahidi unaoonekena, ikikusanya kile wanachokihitajia cha kutengeneza mambo ya Dini yao na dunia yao
  196. Na kwa hakika, utajo wa hii Qur’ani umethibitishwa katika Vitabu vya Manabii waliotangulia, vimeibashiri na kukubali kuwa ni ya kweli
  197. Je, haiwatoshi hawa kuwa ni ushahidi kwamba wewe ni mtume wa Mwenyezi Mungu na kwamba Qur’ani ni kweli kuwa wasomi wa Wana wa Isrāīl wana ujuzi wa usahihi wa hilo na wale walioamini miongoni mwao kama ‘Abdullāh bin Sallām
  198. Na lau tungaliiteremsha Qur’ani kwa baadhi ya wale wasiozungumza lugha ya Kiarabu
  199. wakawasomea makafiri wa Kikureshi kisomo cha Kiarabu kilicho sawa, wangaliikanusha pia na wangalizua sababu ya ukanushaji wao
  200. Hivyo ndivyo tulivyotia ndani ya nyoyo za wahalifu kuikanusha Qur’ani na hilo likawa limejikita ndani ya hizo nyoyo
  201. na hii ikawa ni sababu ya udhalimu wao na uhalifu wao. Basi hapana njia ya wao kubadilika kwa kuyaacha waliyonayo ya kuikanusha Qur’ani mpaka waishuhudie adhabu kali walioahidiwa
  202. Hapo adhabu iwashukie ghafla na hali wao hawajui kuja kwake kabla ya hapo
  203. na hapo waseme, watakaposhtushwa nayo, kwa majuto ya Imani iliyotupita tukaikosa, «Je, sisi ni wenye kupatiwa nafasi na kucheleweshwa tupate kutubia kwa Mwenyezi Mungu ushirikina wetu na tuyapatilize yaliyotupita?»
  204. Je, hawa wamedanganyika na kule kuwapa muhula kwangu ndipo wakawa wanataka kuteremka adhabu kwa haraka juu yao kutoka mbinguni
  205. Je, umejua, ewe Mtume, lau tungaliwastarehesha kwa uhai wa miaka mingi kwa kuwacheleweshea muda wao wa kuishi
  206. kisha iwashukie adhabu ilioahidiwa
  207. Hakutawafaa kitu kule kustarehe kwao kwa umri mrefu na maisha mazuri wasipotubia kutokana na ushirikina wao. Basi adhabu ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuwashukia hivi karibuni (ulimwenguni) au baadaye (huko Akhera)
  208. Na hatukuuangamiza mji wowote, miongoni mwa miji katika mataifa yote, isipokuwa baada ya kuwatumiliza Mitume kwao wawaonye
  209. ili wawe ni makumbusho kwao na uzindushi wa yale yenye uokofu kwao. Na hatukuwa ni wenye kudhulumu kwa kuwaadhibu watu kabla ya kuwapelekea Mtume
  210. Na Qur’ani hawakuiteremsha mashetani kwa Muhammad, kama wanavyodai makafiri
  211. na hilo halifai kutoka kwao na wala hawaliwezi
  212. kwa kuwa wao ni wenye kuzuiliwa kuisikiliza Qur’ani kutoka mbinguni, ni wenye kupigwa na vimondo
  213. Hivyo basi usiabudu, pamoja na Mwenyezi Mungu, muabudiwa yoyote asiyekuwa Yeye, ufanyapo hivyo utateremkiwa na adhabu ile iliyowashukia hawa walioabudu, pamoja na Mwenyezi Mungu, asiyekuwa Yeye
  214. Na watahadharishe, ewe Muhammad, watu wako wa karibu, ukianzia na wale walio karibu na wewe zaidi, isije adhabu yetu ikawashukia
  215. Na uwe laini wa mwenendo na maneno, kwa unyenyekevu na huruma, kwa yule ambaye imekufunukia kutoka kwake kuitika mwito wako
  216. Basi wakienda kinyume na amri yako na wasikufuate, jiepushe na vitendo vyao na yale waliyonayo ya ushirikina na upotevu
  217. Na Umuachie jambo lako Mwenyezi Mungu, Aliye Mshindi Ambaye hakuna wa kushindana na Yeye wala wa kumlazimisha, Mwenye kurehemu Ambaye Hawaachi wenye kumtegemea
  218. Na Ambaye Anakuona unaposimama kuswali ukiwa peke yako ndani ya usiku
  219. Na Anaona vile unavyogeuka, pamoja na wenye kumsujudia katika Swala zao wakiwa na wewe, ukiwa katika hali ya kusimama, kurukuu na kusujudu na kuketi
  220. Hakika Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Anayesikia kusoma kwako na kumtaja kwako, Ndiye Anayejua nia yako na matendo yako
  221. Je, niwapashe habari, enyi watu, ni nani ambaye mashetani wanamshukia
  222. Wanamshukia kila mwingi wa urongo, mwingi wa madhambi miongoni mwa makuhani
  223. Mashetani wanasikiliza kwa kuiba, wanayanyakuwa maneno kutoka sehemu za juu wakawatupia makuhani na wale wanaokuwa na mwenendo wao miongoni mwa watu wenye matendo mabaya. Na wengi wa hawa ni warongo, kwani mmoja wao husema kweli katika neno moja na akaongeza juu yake maneno mia moja ya urongo
  224. Na washairi, mashairi yao yanasimama juu ya ubatilifu na urongo, na wanafuatana na wao wapotevu waliopotoka kama wao
  225. Kwani huoni, ewe Nabii, kwamba wao wanaenda kama mtu aliyekosa mwelekeo, wanavama ndani ya kila aina ya fani za urongo, uzushi, uvunjaji heshima, kutukana nasaba na kuwataja vibaya wanawake waliojihifadhi
  226. na kwamba wao wanayasema wasiyoyatenda, wanapita mipaka katika kuwasifu watu wa ubatilifu na wanawatia kasoro watu wa haki
  227. Mwenyezi Mungu amewavua, kati ya hao washairi, wale washairi walioongoka kwa kuamini na kufanya matendo mema, na wakamtaja Mwenyezi Mungu kwa wingi, wakatunga mashairi juu ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, na kumsifu Yeye, Mwenye utajo mtukufu, na kumtetea Mtume Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wakasema maneno ya busara yenye mawaidha na adabu nzuri, na wakaunusuru Uislamu wakawa wanamtukana anayeutukana au anayemtukana Mtume wake kwa kuwarudi washairi makafiri. Na watajua wale waliozidhulumu nafsi zao kwa ushirikina na matendo ya uasi, wakawadhulumu wasiokuwa wao kwa kuwanyima haki zao au kuwafanyia uadui au tuhuma za urongo, ni marejeo gani ya shari na maangamivu watakayorejea. Kwa kweli, hayo ni mageuko mabaya. Tunamuomba Mwenyezi Mungu salama na afya